1.2. Kifungu cha Kujibu Maswali cha Kwanza Sehemu ya Pili - Maswali

posted Jun 21, 2015, 9:17 PM by Maurice Nyamoti   [ updated Jul 20, 2015, 3:58 AM ]

Soma kifungu kifuatacho kasha ujibu maswali 1-10


Nilizaliwa na kulelewa katika familia iliyotajika. Baba yangu mlajasho alikuwa wa mali na moyo. Mimi na ndugu yangu mdogo hatukujua maana ya uhitaji kwani baba alitukidhia mahitaji yetu yote. Nyumbani mwetu kila siku mlishiba na kutapika watu wa kila sampuli waliokuja kulilia hali kwa baba. Baba aliwasabilia kwa mengi. Kuna waliopewa ruzuku mbalimbali za vyakula, kuna waliopewa vibarua mashambani na waliofanya kazi pale nyumbani. Almuradi kila mwana kijiji alifaidika kutokana na mkono wazi wa baba. Ndugu yangu mdogo hakuisha kuwabughudhi waja hawa na kuwaita waegemea nundu.
Siku zilisonga na kupita kama maji ya mto; hata nikajipata katika shule ya msingi. Niliyakumbatia masomo yangu kwa hamu kubwa. Sikuwa na wakati a kufanya ajizi, kwani baba, pamoja na pato lake nono, hakuwahi kudekeza hisia za ugoigoi. Nasi ilibidi tufuate nyayo zake; kwani mwana akibebwa hutazama kisogo cha nina. Nilifanya mtihani wangu wa darasa la nane na kuvuna nilichopanda. Asubuhi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya mtihani huo, niliamshwa na sauti ya, "pongezi mwanangu," kutoka kwa baba. Baba alikuwa amebeba gazeti la siku hiyo, usoni amevaa tabasamu kubwa. Sikuamini maneno yake, Nilijiunga na shule mojawapo ya kitaifa.
Siku nilipokivuka kizingiti cha lango la shule ya kitaifa ya Tindi ndipo maisha yangu yalipoanza kuingia ufa. Nilikutana na tamasha, mwanafunzi mchangamfu na mcheshi. Alijitambulisha kuwa alisomea shule aliyokuwa jirani na ile yangu ya msingi. Urafiki shakiki ukazaliwa kati yake nami. Tukawa daima tunaandamana. Hayo hayakunitia shaka, kwani Tamasha alinihimiza kila mara nitie masomoni. Hata hivyo, siku zilivyosonga ndivyo tabia yake halisi ilivyonibainikia.
Jioni moja Tamasha alikuja chumbani mangu akiwa amebeba unga aliouita dawa ya homa. Aliniambia nijaribu kutibu homa ambayo ilikuwa imenikaba kwa siku ayami. Nami, kwa kutotaka kumvunja rafiki yangu, nikachukua unga huo na kuutia kinyani; ingawa kwa kweli mwalimu wetu alikuwa ametuonya dhidi ya kutumia dawa zozote bila maelekezo ya daktari. Unga huu haukuitibu homa yangu, ila ulinipa utulivu mkubwa wa akili, utulivu ambao sikuwa nimewahi kuushuhudia maishani.
Tamasha alifika chumbani mwangu usiku kunijulia hali. Alinipata nimejituliza juu ya kitanda changu. Alinisalimu na kukenua kama aliyetarajia jawabu fulani kutoka kwangu. Nilimweleza hali yangu naye akaniambia kuwa hivyo ndivyo dawa hiyo ifanyavyo kazi; kwamba amekuwa akiitumia kwa muda, hata nyakati za mtihani ; naye  hupata nguvu za kukabiliana na majabali yote. Alielekeza kwa mzee Kamaliza ambaye ndiye aliyekuwa akimuuzia unga huo. Kuanzia siku hiyo nikawa mteja mwaminifu wa Kamaliza. Nilitumia unga huu bila fikira nikidhani kuwa ilikuwa dawa ya homa tu! Sikujua ilikuwa dawa ya kulevya; na Tamasha alikuwa mraibu sugu wa dawa hiyo na nyingine nyingi "uzuri wake huu ni wa mkakasi tu?" Nilijiuliza. "Laiti ningalijua". Hata hivyo maswali yote haya hayakuwa na faida tena. Nilikuwa tayari nimezama katika tatizo sugu lamatumizi ya dawa za kulevya.
Nilijisuta moyoni kwa matumizi ya dawa za kulevya ambayo yalielekea kuyagongesha mwamba maisha yangu shuleni. Hata hivyo, haikuwa rahisi kuacha kwani nilichelea kuitwa limbukeni na wenzangu. Matokeo ya haya yote yakawa kuzorota kwa masomo yangu. Walimu hawakuchelewa kuona mabadiliko yaliyonikumba. Walijaribu kunishauri na kutaka kujua kilichokuwa kikinisumbua. Walipoona kwamba hali yangu haibadiliki na kwamba nimeshindwa kuwaambia tatizo langu, walimjulisha mwalimu mkuu ambaye hakukawia kumwita baba.
Mazungumzo kati ya baba na mwalimu mkuu yalinitia fadhaa kubwa kwani sikutaka kuwaambia nilitumia dawa za kulevya; ingawa kwa kweli mwalimu mkuu alishuku. Walijaribu kunishika sikio kuhusiana na tabia hii yangu; lakini tangu lini sikio la kufa likasikia dawa? Niliendelea na uraibu angu hadi siku nilipofunzwa na ulimwengu baada ya kufumaniwa na naibu wa mkuu wa shule mjini nikipiga maji. Nilipewa adhabu niliyotarajia. Nilijipata nyumbani kwa muda wa mwezi mzima, nikiuguza vidonda vya moyo na akili. Kijiji kizima kilijua nimefukuzwa shule kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya. Sikuwa na pa kuutia uso wangu. Hata hivyo hili lilikuwa tunzo kubwa kwangu
Mama yangu aliweza kunipa nasaha na kunishauri niache dawa hizo. Mara hii, maneno aliyoniambia yalikuwa na maana. Niliyasikiliza kwa makini. Hata baba alipopata barua kumwarifu aniregeshe shule, nilikuwa tayari kurudi na kuyaanza maisha upya. Nilikuwa nimeamua kujiunda na chama cha vijana wanaopigana na matumizi mabaya ya dawa shuleni.

 1. Mambo yanayoonyesha kuwa mlajasho alikuwa tajiri wa mali na moyo ni:
  1. Kukidhi mahitaji ya wana, watu kumlilia hali
  2. Kukidhi mahitaji ya wana, kuwapa watu riziki
  3. Kukidhi mahitaji ya wana, kumkanya mwanawe
  4. Kukidhi mahitaji ya wana, watu kumfuata kwake
 2. "Ndugu yangu mdogo hakuisha kuwabughudhi waja hawa na kuwaita waegeea nundu" inaonyesha kuwa ndugu mdogo alikuwa
  1. mwenye uzushi
  2. mwenye kulisifu
  3. mwenye mapuuza
  4. mwenye uchoyo
 3. Msimulizi alisoma kwa hamu kwa kuwa
  1. alipenda masomo yake
  2. baba yake alikuwa mkali
  3. baba yake alikuwa mwenye bidii
  4. alitaka kufuata nyayo za ndugu yake
 4. Kifungu "ndipo maisha yangu yalipoanza kuingia ufa" kinamaanisha:
  1. Maisha ya msimulizi yalianza kupata matatizo
  2. maisha ya msimulizi yaliporomoka
  3. maisha ya msimulizi yalianza kubadilika
  4. maisha ya msimulizi yaliharibika
 5. Msimulizi hkutaka kuacha "unga" kwa sababu:
  1. alikuwa amezoea uraibu wa Kamaliza
  2. hakutaka kumuudhi Tamasha
  3. alichelea kuondolewa kundini na wenzake
  4. alichelea kudunishwa na wenzake
 6. Mambo yanayoonyesha kuwa Kifungu hiki kinapinga matumizi ya dawa za Kulevya ni:
  1. msimulizi kufukuzwa shule, msimulizi kujiunga na wanaopinga mabaya ya dawa shuleni
  2. wlaimu kushauri msimulizi, mama pamoja na mwalimu mkuu kumwonya msimulizi shuleni.
  3. kamaliza kuacha kuuza dawa, mama kumshauri msimulizi
  4. walimu kugundua tatizo la msimulizi, msimulizi kuaibika shuleni
 7. Kulingana na kifungu hiki, jamii inakabiliana na tatizo la matumizi mabaya ya dawa kwa:
  1. kuwapeleka watoto shuleni, matajiri kuwasaidia watu
  2. ushirikiano kati ya wazazi na walimu, kuwajibika kwa vijana
  3. ushirikiano kati ya wazazi na walimu, kuaibika kwa vijana
  4. wazazi kwenda shuleni wanapoitwa, kuwajibika kwa vijana
 8. Methali amboayo haifai kujumliisha ujumbe wa taarifa hii ni:
  1. nazi mbovu harau ya nzima
  2. mchezea tope humrukia
  3. mwegemea nundu haachi kunona
  4. mchovya asali hachovyi mara moja
 9. "uzuri wake huu ni wa mkakasi tu?" ina maana Tamasha:
  1. alikuwa mcheshi
  2. alikuwa mnafiki
  3. hakuweza kuaminika
  4. hakuweza kutegemewa
 10. Msimulizi alikuwa "sikio la kufa" kwa sababu:
  1. hakupona homa baada ya kutumia unga
  2. hakuacha uraibu wake baada ya kuonywa na baba na mwalimu
  3. alifumaniwa na naibu wa mwalimu mkuu akipiga maji
  4. alipata adhabu aliyotarajia baada ya kupiga maji
fasihi