1.6. Kifungu cha Kujibu Maswali cha Kwanza Sehemu ya Sita - Maswali

posted Jun 21, 2015, 9:17 PM by Maurice Nyamoti   [ updated Jul 20, 2015, 4:16 AM ]

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 1-10


Hatua ya serikali ya Uingereza kuwalipa fidia Wakenya walioteswa na serikali ya wakoloni ilipokabiliana na wapiganaji wa       Maumau  haifai kushangiliwa  jinsi baadhi ya watu wanavyofanya. Inasikitisha kwamba baadhi ya watu wanasifu hatua hiyo bila kuzingatia masaibu waliyopitia wapiganaji hao ambayo yanawaandama hadi wakati huu.

          Kitita cha shilling billion mbili nukta sita ambacho serikali hiyo ilitoa  kwa wapiganaji elfu tano walioshtaki Uingereza kupitia kwa tume ya haki za kibinadamu  ya Kenya ni kama dharau kwa wapiganaji hao. Watakaonufaika na fidia hiyo ni walionusurika kifo wakati wenzao waliuawa. Ni wale waliotumbukizwa vizuizini wakahasiwa na makovu ya dhuluma hizo yatadumu milele. Dhuluma hizo zilikuwa  za kinyama kiasi kwamba hakuna kiwango cha pesa kinachoweza kuzifidia. Kwamba serikali ya Uingereza iliamua kusuluhisha kesi hiyo  nje ya mahakama ni ishara kwamba ilikuwa na hakika mahakama ingewapa wapiganaji hao fidia kubwa.

          Maovu ambayo wapiganaji wa Mau Mau walipitia kwa ajili ya nchi hii ni mengi. Kweli walikata pua ili waunge wajihi. Serikali inafaa kuwatambua na kuhakikisha kwamba baadhi yao wakilala bila chakula na kuishi katika mabanda sawa na ilivyokuwa walipopambana na wakoloni  kukomboa nchi hii ambayo wanasiasa  wanafurahia. Katika mila za Kiafrika  ,ni laana kumpuuza mtu aliyemwaga damu kwa ajili yako na kutowajali wapiganaji hao huenda kumesabibisha hai ilivyo katika nchi hii ambapo maovu yanazidi kukolea  huku maadili yakiendelea kumomonyoka.

          Wazee walioingia msituni kupigania nchi hii na akina mama walioteswa  wakidaiwa kuhusika na wapiganaji hao wanastahili fidia ya kutosha. Serikali ya uingereza iliwachezea shere  wapiganaji hao kama ilivyozoea kufanya katika mambo mengi. Kumbuka Uingereza ingali katika dhana potovu kuwa Mwafrika  hawezi kujiamulia shida zake. Wakae wakijua kuwa mjinga akierevuka mwerevu yu mashakani.

          Hata hivo ifahamike kuwa,kusema haya siwachochei wapiganaji hao kukataa pesa hizo zilizotolewa,ila ninashawishika kwa dhati kuwa mengi yalihitajika kufanywa. Badala ya kukimbilia   hela chache kama hizo,ingekuwa bora kama Uingereza ingeanzisha wakfu maalum wa kuwatunza Wanamaumau hao,kuwasomesha wana wao,kuwajengea makao na kuhakikisha wanaishi  maisha mema. Kwa kuanzisha wakfu huo na kutenga pesa za kushughulikia kila  mwaka,kungewafaidi wakongwe hao ambao baadhi yao wanaugua  vidonda  vya moyo visivyoponyeka kwa hela chache bali kwa haki.

          Katika suala hili, serikali ya Uingereza ilijitia kitanzi. Sasa sina shaka kwamba,kwa kufidia wapiganaji  hao,Uingereza ilifungua mlango kwa madai kama hayo kutoka pembe zote za dunia ambako watawala wake walitekeleza maovu chini ya ukoloni.


1.    Kulingana na aya ya kwanza,__

a.       Mwandishi anafurahia hatua ya serikali ya Uingereza kulipa fidia.

b.    Wakenya walioteswa na serikali ya mkoloni hawakulipwa chochote.

c.     Mwandishi hajafurahia fidia iliyolipwa na serikali ya Uingereza kwa wapiganaji  wa Maumau.

d.    Serikali ya Uingereza ilizingatia  masaibu  ambayo Mau Mau walipitia katika kulikomboa taifa hili. 

2.    Wapiganaji wa Maumau walitumia njia gani kuwasilisha malalamiko yao?

a.     Tume ya katiba na maswala ya haki nchini

b.    Tume ya haki za kibinadamu ya Kenya

c.     Wapiganaji wa Mau mau  ambao waliuliwa

d.    Tume ya maridhiano na haki za kibinadamu nchini Uingereza

3.    Kulingana na makala haya, kitita cha shilingi billioni  mbili nukta sita__

a.     Ni kiasi kidogo sana kikilinganishwa na dhuluma walizopitia Wanamaumau

b.    Ni kiasi kikubwa sana cha pesa kwa kuwa si wengi hulipwa kiasi hicho cha pesa

c.     Ni kiasi kikubwa sana cha pesa kikilinganishwa na masaibu ya Wanamaumau.

d.    Ni kiasi cha pesa ambacho hakipaswi kupuuzwa na Mkenya mwenye masaibu.

4.    Kweli walikata pua ili waunge wajihi. Hii ina maana kuwa___

a.     Wakoloni wengi walinyanyasa wakenya  kwa kuzikata pua zao.

b.    Wanamaumau walishiriki katika vita ambavyo ingawa viliwahasiri vililetea taifa hili manufaa ya uhuru.

c.     Wanamaumau waliamua kuzikata pua zao ili kuonyesha kero kwa serikali ya mkoloni

d.    Sura za wakenya wengi zilikuwa  mbaya hususani kwa kuwa na pua ndefu.

5.    Kwa maoni ya mwandishi,maadili yanazidi kumomonyoka___

a.     Baadaya vijana kupuuza mawazo ya wakubwa wao

b.    Kwa kuwa siku hizi walimu na wazazi wamekwepa majukumu yao ya ulezi

c.     Kwa sababu ya mashindano makali baina ya jinsia ya kike na ile ya kiume

d.    Kwa kupuuza mchango wa wale waliomwaga damu na kuupigania uhuru wa Wakenya.

6.    Fidia ni malipo yapi?

a.     Yanayolipwa mtu baada ya kuhusika katika ajali

b.    Malipo kwa ajili ya hasara

c.     Ni yale yanayolipwa aliyechafuliwa sifa

d.    Ya kuingia vitani

7.    Katika mwanzo wa aya ya nne,neon ‘wazee’ limetumika kwa maana ya__

a.     Wote walioingia msituni kupigana na serikali mkoloni.

b.    Wanaume na wanawake waliokula chumvi  nyingi.

c.     Wanaume waliobugia chumvi nyingi.

d.    Wote waliochangia kupigana na serikali ya mkoloni

8.    Ni nini maana ya ‘kuchezea shere’

a.     Kunyanyasa

b.    Kudhulumu

c.     Kuhadaa

d.    Kupendelea

9.    Kwa maoni ya mwandishi, suluhisho la kudumu lingekuwa__

a.     Kuongeza kiasi cha pesa iliziweze kukidhi mahitaji ya kila Mwanamaumau

b.    Kuanzisha wakfu wa kuwafaa Wanamaumau wakati wataabu

c.     Kuhakikisha kuwa serikali ya Uingereza imeomba msamaha kwa dhuluma ilizowafanyia Wanamaumau

d.    Kukataa kuchukua pesa zozote kutoka kwa serikaliya Uingereza.

10.   Kauli inayosimamia makala haya ni kuwa__

a.     Fidia ni bora lakini wakfu ni bora  zaidi

b.    Fidia ni bora kuliko wakfu

c.     Wakfu ni bora kwa kuwa hauhitaji pesa zozote

d.    Fidia ni bora sawa na wakfu lakini fidia ni bora zaidi

fasihi