1.0. Kifungu cha Kujibu Maswali Sehemu Nunge - Maswali

posted Jun 21, 2015, 9:05 PM by Maurice Nyamoti   [ updated Jul 20, 2015, 3:53 AM ]

Soma kifungu kifuatacho kasha ujibu maswali 1-10.


Hatua ya serikali ya Uingereza kuwalipa fidia Wakenya walioteswa na serikali ya wakoloni ilipokabiliana na wapiganaji wa maumau haifai kushangiliwa jinsi baadhi ya watu wanavyofanya. Inasikitisha kwamba baadhi ya watu wanasifu hatua hiyo bila kuzingatia masaibu waliyopitia wapiganaji hao ambayo yanawaandama hadi wakati huu.
Kitita cha shillingi bilioni mbili nukta sita ambacho serikali hiyo ilitoa kwa wapiganaji elfu tano walioshataki Uingereza kupitia kwa tume ya haki za binadamu ya Kenya ni kama dharau kwa wapiganaji hao. Watakaonufaika na fidia hiyo ni walionusurika kifo wakati wenzao waliuawa. Ni wale waliotumbukizwa vizuizini wakahasiwa na makovu ya dhuluma hizo yatadumu milele. Dhuluma hizo zilikuwa za kinyama kiasi kwamba hakuna kiwango cha pesa kinachoweza kuzifidia. Kwamba serikali ya Uingereza iliamua kusulusisha kesi hiyo nje ya mahakama ni ishara kwamba ilikuwa na hakika mahakama ingewapa wapiganaji hao fidia kubwa.
Maovu ambayo wapiganaji wa Mau Mau walipitia kwa ajili ya nchi hii ni mengi. Kweli walikata pua ili waunge wajihi. Serikali inastahili kuwatambua na kuhakikisha kwamba baadhi yao wakilala bila chakula na kuishi katika mabanda sawa na ilivyokuwa walipopambana na wakoloni kukomboa nchi hii ambayo wanasiasa wanafurahia. Katika mila za Kiafrika, ni laana kumpuuza mtu aliyemwaga damu kwa ajili yako na kutowajali wapiganaji hao huenda kumesababisha hali ilivyo katika nchi hii ambapo maovu yanazidi kukolea huku maadili yakiendelea kumomonyoka.
Wazee walioingia msituni kupigania nchi hii na akina mama walioteswa wakidaiwa kuhusika na wapiganaji hao wanastahili fidia ya kutosha. Serikali ya Uingereza iliwachezea shere wapiganaji hao kama ilivyozoea kufanya katika mambo mengi. Kumbuka Uingereza ingali katika dhana potovu kuwa Mwafrika hawezi kujiamulia shida zake. Wakae wakijua kuwa mjinga akierecuka mwerevu yu mashakani.
Hata hivyo, ifahamike kuwa, kwa kusema haya siwachochei wapiganaji hao kukataa pesa hizo zilizotolewa, ila ninashawishika kwa dhati kuwa mengi yalihitajika kufanywa. Badala ya kukimbilia hela chache kama hizo, ingekuwa bora kama Uingereza ingeanzisha wakfu maalumu wa kuwatunza wanaMauMau hao, kuwasomesha wana wao, kuwajengea makao na kuhakikisha wanaisha maisha mema. Kwa kuanzisha wakfu huo na kutenga pesa za kuushughulikia kila mwaka, kungewafaidi wakongwe hao ambao baadhi yao wanaugua vidonda vya moyo visivyoponyeka kea hela chache bali kwa haki.
Katika suala hili, serikali ya Uingereza ilijitia kitanzi. Sasa sina shaka kwamba, kwa kufidia wapiganaji hao, Uingereza ilifungua mlango kwa madai kama hayo kutoka pembe zote za dunia ambako watatawala wake walitekeleza maovu nchini ya ukoloni.

1. Kulingana na aya ya kwanza,
A. Mwandishi anafurahia hatua ya serikali ya Uingereza kulipa fidia
B. Wakenya walioteswa na serikali ya mkolomi hawakulipwa chochote
C. Mwandishi hajafurahia fidia iliyolipwa na serikali ya Uingereza kwa wapiganaji wa MauMau
D. Serikali ya Uingereza ilizingatia masaibu ambayo MauMau walipitia katika kulikomboa taifa hili
2. Wapiganaji wa MauMau walitumia njia gain kuwasilisha malalamiko yao?
A. Tume ya katiba na maswala ya haki nchini
B. Tume ya haki za binadamu ya Kenya
C. Wapiganaji wa MauMau ambao waliuliwa
D. Tume ya maridhiano na haki za kibinadamu nchini Uingereza
3. Kulingana na makala haya, kitita cha shilingi bilioni mbili nukta sita
A. Ni kiasi kidogo sana kikilinganishwa na dhuluma walizopitia wanaMauMau ambao waliuliwa
B. Ni kiasi kikubwa sana cha pesa kwa kuwa si wengi hulipwa kiasi hicho cha pesa
C. Ni kiasi kikubwa sana cha pesa kikillinganishwa na masaibu ya WanaMauMau
D. Ni kiasi cha pesa ambacho hakipaswi kupuuzwa na mkenya mwenye masaibu
4. Kweli walikata pua ili waunge wajihi. Hii ina maana kuwa
A. Wakoloni wengi walinyanyasa waKenya kwa kuzikata pua zao
B. WanaMauMau walishiriki katika vita ambavyo ingawa viliwahasiri vililetea taifa hili manufaa ya uhuru
C. Wanamaumau waliamua kuzikata pua zao ili kuonyesha kero kwa serikali ya mkoloni
D. Sura za Wakenya wengi zilikuwa mbaya hususan kwa kuwa na pua ndefu
5. Kwa maoni ya mwandishi, maadili yanazidi kumomonyoka
A. Baada ya vijana kupuuza mawazo ya wakubwa wao
B. Kwa kuwa siku hizi walimu na wazazi wamekwepa majukumu yao ya ulezi.
C. Kwa sababu ya mashindano makali baina ya jinsia ya kike na ile ya kiume
D. Kwa kupuuza mchango wa wale waliommwaga damu na kuupigania uhuru wa Wakenya
6. Fidia ni malipo yapi?
A. Yanayolipwa mtu baada ya kuhusika katika ajali
B. Malipo kwa ajili ya hasara
C. Ni yale yanayolipwa aliyechafuliwa sifa
D. Ya kuingia vitani
7. Katika mwanzo wa aya ya nne, neon Wazee limetumika kwa maana ya
A. Wote walioingia msituni kupigana na serikali mkoloni
B. Wanaume na wanawake waliokula chumvi nyingi
C. Wanaume waliobugia chumvi nyingi
D. Wote waliochangia kupigana na serikali ya mkoloni
8. Ni nini maana ya ‘kuchezea shere’
A. Kunyanyasa
B. Kudhulumu
C. Kuhadaa
D. Kupendelea
9. Kwa maoni ya mwandishi, suluhisho la kudumu lingekuwa:-
A. Kuongeza kiasi cha pesa ili ziweze kukidhi mahitaji ya kila mwanaMauMau
B. Kuanzisha wakfu wa kuwafaa wanaMauMau wakati wa taabu
C. Kuhakikisha kuwa serikali ya Uingereza imeomba msamaha kwa dhuluma ilizofanyia wanaMauMau
D. Kukataa kuchukua pesa zozote kutoka kwa serikali ya Uingereza
10. Kauli inayosimamia makala haya ni kuwa
A. Fidia ni bora lakini wakfu ni bora zaidi
B. Fidia ni bora kuliko wakfu
C. Wakfu ni bora kwa kuwa hauhitaji pesa zozote
D. Fidia ni bora sawa na wakfu lakini fidia ni bora zaidi

1.0. Kifungu cha Kujibu Maswali Sehemu Nunge - Majibu [you need to sign in first and to sign in, you must be a member]
1.1. Kifungu cha Kujibu Maswali Sehemu ya Kwanza - Maswali
Nyuma

fasihi