2.3. Kifungu cha Kujibu Maswali cha Pili Sehemu ya Tatu - Maswali

posted Jun 21, 2015, 9:17 PM by Maurice Nyamoti   [ updated Jul 20, 2015, 7:01 AM ]

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 1-10


Mojawapo ya maswali yanayomshugulisha binadamu tangu zamani ni asili au chimbuko la lugha mbalimbali zilizoenea ulimwenguni. Hamu hiyo hutokana na uwezo mkubwa na muujiza unaofumbatwa na lugha yoyote ile. Baadhi ya maelezo yanayotolewa na wajuzi ni yenye utaalamu mkubwa.
Kiswahili ni lugha tunayoionea fahari hapa Afrika Mashariki. Inaamini kuwa lugha hii ilizungumzwa kwa mara ya kwanza katika pwani ya Afrika Mashariki na hasa ipande wa kaskazini wa pwani ya Kenya. Lugha hii ni kiungo muhimu ambacho ni msingi wa muungano wetu na inatuwezesha kujitambulisha kama watu wa eneo hili. Aidha, lugha hii ni nyenzo muhimu inayounganisha pamoja, kama gundi, watu wa makabila mbalimbali pasi na kuwazia jadi wala nasaba zao. Kwa njia hii lugha hii inayarahisisha mawasiliano baina ya watu wenye asili, rangi na utaifa tofauti. Je, ushawahi kuliwazia chimbuko la ligha hii muhimu?
Zipo nadharia zinazotolewa kuelezea asili ya lugha hii. Moja wapo ya nadharia hizo ni ile inayoiona lugha hii kama lugha ya mseto. Kwa msingi wake, lugha ya Kiswahili ni zao la kuingilia kwa lugha za kigeni kama Kihindi, Kiarabu, Kiajemi na lugha za makabila ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki. Walioishikilia nadharia hii walidai kuwa vitoto vya watu walioingiliana kutoka jamii mbalimbali viliishia kuzungumza Kiswahili. Udhaifu wa nadharia hii unatokana na kuwa inaegemea kwenye kipimo kimoja tu: msamiati. Ni kweli kuwa Kiswahili kina maneno ya Kihindi (kama chapatti, laki na bima), ya Kiajemi (kama darubini, maridadi na desturi), ya Kijerumani (kama shule) nay a lugha nyinginezo. Lakini kipimo cha msamiati pekee hakitoshi kuichunguzia lugha. Lazima muundo wa sentensi na sifa nyinginezo kama sauti zichunguzwe.
Nadharia nyingine ambayo pia ina udhaifu ni ile inayoiona lugha ya Kiswahili kama tokeo la ndoa baina ya wanawake wa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu. Wanaoishikilia wanasema kuwa watoto walozaliwa walizungumza Kiswahili! Wafuasi wa nadharia hii wanatumia kigezo msamiati mwingi katika lugha ya Kiswahili kuwa wa Kiarabu. Hata hivyo, pana uwezekano gani? Kwa mfano, wa mtu mwenye asili ya Marakwet na Mdigo kuoana na kasha mtoto wao aongee lugha ngeni?
Nadharia ambayo inakubalika na wengi ni kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha ya Kibantu. Nadharia hii inatumia ushahidi wa kiisimu, yaani wa sayansi ya lugha, na kihistoria. Wataalamu hawa wanaichunguza lugha hii pamoja na lugha zinazojulikana kama za kibantu na kuonyesha uhusiano wake. Mtaalamu maarufu anayehusishwa na nadharia hii anajulikana kama Malcom Guthrie. Mtaalamu huyu mwenye asili ya nchi ya Uingereza, alichukua kipindi cha miaka takribani 20 kuukamilisha uchunguzi wake. Guthrie alichunguza uhusiano uliopo baina ya lugha za Kibantu katika maeneo yanayokaliwa na watu wanaofahamika kama Wabantu. Watu hao wanapatikana katika eneo lililoko kusini mwa Jangwa la Sahara kuanzia maeneo ya Kameruni, Afrika ya Kati, Afrika ya Kusini na Afrika Mashariki.

1. Kwa mujibu wa maneno ya ufunguzi katika ufahamu:-
a. Maswali kuhusu chimbuko la Kiswahili hayamshughulishi binadamu
b. Hakuna maswali yanayomshughulisha binadamu isipokuwa kuhusu chimbuko la Kiswahili
c. Kati ya maswali mengine, linalohusu chimbuko la Kiswahili linamshughulisha binadamu
d. Maswali mengi yanamshughulisha binadamu lakini lili la chimbuko la Kiswahili si moja la hayo
2. Mwandishi angetumia neon gani msemo “tunayoionea fahari” ?
a. Tunayoidhamini
b. Tunayoidunisha
c. Tunayoidumisha
d. Tunayoienzi
3. Zifuatazo ni athari bora za lugha ya Kiswahili isipokuwa gani? Ni lugha:-
a. Inayochochea ukabila
b. Inayowaleta watu pamoja
c. Inayorahisisha mawasiliano
d. Inayowatambulisha watu wa Afrika Mashariki
4. Mwandishi anamaanisha nini kwa kutumia maneno ‘lugha ya mseto’? Lugha:-
a. Inayofanyiwa na lugha za kigeni tu
b. Isiyotia ndani athati ya lugha za kigeni
c. Ambayo na mchanganyiko wa lugha hata za kigeni
d. Ambayo haieleweki ilitoka wapi
5. Nadharia kwamba Kiswahili ni lugha ya mseto ina udhaifu gani?
a. Inatumia maneno ya kigeni
b. Inaeleza msamiati usioweza kuunda sentensi
c. Haijaichunguza lugha ya Kiswahili kwa vyovyote.
d. Haijachunguza mengi kukihusu Kiswahili ila msamiati tu.
6. Nadharia inayosema kuwa Kiswahili ni tokeo la ndoa, inaeleza kuwa mswahili ni:-
a. Mwanamke wa pwani na mwarabu
b. Mtoto wa mwanamke wa pwani au mwarabu
c. Mwanamke mpwani aliyeolewa na mwarabu
d. Mtoto wa mwarabu na mwanamke mpwani
7. Ni nini kinachoshangaza kuhusu Kiswahili kuitwa lugha iliyotokana na ndoa
a. Jinsi ilivyowezekana mwarabu kuoa mwafrika
b. Jinsi ilivyowezekana mtoto wa kabila Fulani kuzaliwa na kuongea lugha tofauti
c. Jinsi ilivyowezekana Kiswahili kuwa maarufu kuliko Kiingereza
d. Jinsi ilivyowezekana msamiati wa kiarabu kuingizwa kwenye Kiswahili
8. Ni nadharia ipi inayokubalika na wengi kwamba inaelezea chimbuko la Kiswahili
a. Kiswahili ni lugha ya kibantu
b. Kiswahili ni tokeo la ndoa
c. Kiswahili ni lugha ya kigeni
d. Kiswahili ni lugha ya mseto
9. Mtaalamu Malcom Guthrie alichukua muda gani kufanya uchunguzi wake?
a. Miaka ishirini kamili
b. Miaka ishirini hivi
c. Chini ya miaka ishirini
d. Zaidi ya miaka ishirini
10. Kipi si kichwa mwafaka kwa habara uliyoisoma?
a. Chimbuko la Kiswahli
b. Umuhimu wa Kiswahili
c. Asili ya Kiswahili
d. Chanzo cha Kiswahili

KISWAHILI PAST PAPERS