2.4. Kifungu cha Kujibu Maswali cha Pili Sehemu ya Nne - Maswali

posted Jun 21, 2015, 9:17 PM by Maurice Nyamoti   [ updated Jul 20, 2015, 7:15 AM ]

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali 1-10


Kiprono anakumbuka kidogokidogo mambo yaliyotokea. Ng’ombe walipoanza kunyanyua vichwa vyao na kutapatapa ndipo alipoona moshi upande wa mashariki, alikokuwa ameenda Nyatichi.
Alikimbilia huko na tawi la mti. Alianza kuuzima moto kwa ari na idili. Alikuwa yup eke yake wakati huo na kama Waswahili walivyonena, ‘kidole kimoja hakivunji chawa.’ Kwa hiyo punde si punde moto ule ulianza kumchachafya. Bidii yake haikufua dafu asilani. Aliona amezungukwa na adui ambaye kwa kweli kumshinda kulihitaji uwezo kuliko aliokuwa nao.
Alitupa tawi lake la kuuzima moto na kuanza kupiga kamsa, ‘’moto! Moto!’’ Moshi ulikuwa umemwingia machoni na kufanya asiweze kuona vizuri. Kiprono alikimbia pasi kujua ni upande upi aliokuwa akienda. Alihemahema na kusepetuka kama mlevi. Lakini aliendelea kukimbia tu na kuomba msaada.
Hata hivyo, nguvu zake zilikuwa zimedidimia. Kiprono ni kijana mwenye nguvu, lakini sulubu alaiyoifanya kuuzima moto peke yake ilimwacha mnyonge kupindukia. Alifika katika barabara moja kuu iendayo mjini. Akasimama. Mbele kulikuwa hakuendeki. Ulikuwa ukomo wa mbio zake. Alitaka kwenda akashindwa. Alianguka ghafla na kuzirai palepale barabarani.
Ndiposa walipokuja watalii Fulani na gari lao wakaona kijana mwanaume amelala chali barabarani. Walisimamisha gari lao wakatoka na kumkagua. Alikuwa anapumua kidogokidogo. Mwili wake ulikuwa na joto jingi. Shati lake alikuwa kalitupilia mbali. Walibaini kuwa alikuwa taabani, si wa maji si wa chakula. Wakamwonea imani na kumbeba na kumweka garini, wakampeleka hospitalini mjini Kapsara.
Alipofikishwa hospitalini alikuwa hajijui hajitambui. Wahisani wake walimwacha amelazwakitandani, wakaendelea na safari yao. Walikuwa wakienda kwenye mbuga ya kuhifadhi wanyama ya Maasai Mara.
Kama walivyosema wahenga, ‘‘kuregarega si kuoza matumbo na kuugua si kufa’’. Baada ya majuma mawili, Kiprono alipata fahamu yake. Aligutuka sana kujipata kitandani. Kulia na kushoto kulikuwa na safu ya vitanda vya wagonjwa wa kila aina. Alimaka. Hakujua pale alifika vipi, wala hakujua kule nyuma atokako yapi yaliyokuwa yametokea.
Kichwa kilikuwa kinamuuma alipogutuka kutoka katika usingizi huo mrefu. Alitaka kujipindua lakini akashindwa. Mwili mzima ulikuwa mzito na mchovu kwelikweli. Alihisi kitefutefu. Kisha yakamtoka matapishi pale kitandani. Aliona muuguzi yuaja kwa mbali. Halafu akawa haoni tena, zikiwa zimempotea fahamu

1. Kwa nini ng’ombe qwaliinua vichwa na kutapatapa ?
a. Walimwogopa Nyatichi rafikiye Kiprono
b. Ilikuwa ishara ya kushiba
c. Walisakamwa na moshi uliovuka
d. Walifurahia joto la moto uliowaka
2. Unafikiri mwandishi angetumia methali gani badala ya ‘kidole kimoja hakivunji chawa’?
a. Ukitaka cha mvunguni sharti uiname
b. Haba na haba hujaza kibaba
c. Juhudi ni pato
d. Kofi halilii kwa kiganja kimoja
3. Kwa nini Kiprono alitupa tawi lake la kuuzima moto na kuanza kupiga kamsa?
a. Alikuwa amepiga moyo konde kuuzima moto
b. Alikuwa amekula yamini kuuzima moto
c. Alikuwa ameinua mikono kwa kushindwa na moto
d. Alikuwa ametaka kamba kwa kushindwa na moto
4. Kwa nini mwandishi ametumia neon ‘sulubu’ kueleza kazi ya kuzima moto aliyoifanya Kiprono?
a. Ilikuwa kazi ya mtu mmoja
b. Ilikuwa kazi ngumu sana
c. Ilikuwa kazi ya kujitolea
d. Ilikuwa kazi rahisi
5. Kiprono alipoifikia barabara moja kuu iendayo mjini, kwa nini mbele kulikuwa hakuendeki
a. Mjini kulikuwa mbali mno na hakuwa na gari
b. Moto mkubwa uliowaka uliizuia njia
c. Ilikuwa barabara ya watalii na Kiprono hakuwa mtalii
d. Alikuwa ameishiwa na nguvu za kuendelea na safari
6. Watalii walimpata Kiprono amejilaza namna gani?
a. Ubavu mmoja chini
b. Tumbo chini
c. Tumbo juu
d. Mgongo juu
7. Mambo yote haya yaliwasaidia watalii kujua kwamba Kiprono alikuwa taabani isipokuwa gani?
a. Hakuwa na maji wala chakula
b. Hakuwa amevalia shati
c. Alipumua kidogokidogo
d. Mwili wake ulikuwa na joto jingi
8. Kwa nini Kiprono aligutuka alipojipata kitandani, hospitalini?
a. Hakujua jinsi gani au kwa nini alikuwa pale
b. Alishtuka kuona amezungukwa na wagonjwa
c. Alikuwa bado hajarudiwa na fahamu
d. Maumivu ya moto yalimkaba na kumgutusha
9. Neno ‘muuguzi limepigiwa mstari katika habari. Linamrejelea nani?
a. Daktari aliyekuwa akimtibu Kiprono
b. Mtu aliyemtunza Kiprono na wagonjwa wengine
c. Mgonjwa mwengine aliyekuwa ameugua kwa moto
d. Mja aliyekuwa amemwunguza Kiprono kwa moto
10. Habari uliyoisoma inazungumzia jinsi Kiprono alivyopambana na kuathiriwa na____moto
a. Tanuri ya
b. Gharika ya
c. Biwi la
d. Wingu la

fasihi